Friday, 24 October 2025

Mgombea Udiwani Erasto Mpete Aahidi Maendeleo kwa Wananchi wa Nole, Kata ya Utalingolo

 













NNa Mwandishi wetu

Oktoba 23, 2025  Mgombea udiwani wa Kata ya Utalingolo, Ndugu Erasto Mpete, ameahidi kuwaletea wananchi wa  Nole maendeleo ya kweli endapo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao endapo watamchagua.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliokusanyika kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika tarehe 23 Oktoba, Ndugu Mpete alisema dhamira yake kuu ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kujituma, akisisitiza kuwa ataweka kipaumbele katika sekta za elimu, afya, kilimo, umeme, na usafi wa mazingira.


 “Ninawaomba mnitume mimi, mtoto wenu, niwaletee maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Nole. Hayo ndiyo maeneo nitakayoanza nayo mara baada ya kupata ridhaa yenu,” alisema Mpete huku akishangiliwa na wananchi.

Mgombea huyo aliongeza kuwa maendeleo ni mchakato unaohitaji uvumilivu na ushirikiano wa wananchi wote, akihimiza umoja na ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 “Tuamini kwamba maendeleo si jambo la siku moja. Ni safari inayohitaji ushirikiano, mipango thabiti, na uongozi makini,” alisisitiza.


Mwisho wa hotuba yake, Ndugu Mpete aliwataka wananchi wa Kata ya Utalingolo kujitokeza kwa wingi tarehe 29, siku ya uchaguzi mkuu, na kupiga kura kwa amani, upendo, na umoja, kwa wagombea wanaowaamini kuwa watatetea maslahi ya wananchi.


Wednesday, 22 October 2025

Mahenge Aahidi Kuleta Maendeleo Endelevu Kata ya Mji Mwema














Njombe, Oktoba 2025 — Mgombea Udiwani wa Kata ya Mji Mwema kupitia Halmashauri ya Mji Njombe, Ndugu Nestory Mahenge, ameahidi kuleta mabadiliko chanya na ya kweli katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi, ikiwemo elimu, maji safi na salama, pamoja na afya bora kwa wote.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mji Mwema, Ndugu Mahenge alisema kuwa ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi wa kata hiyo ananufaika na huduma bora za kijamii bila upendeleo.

> “Ninaamini maendeleo ya kweli yanaanza na elimu bora kwa watoto wetu, maji safi kwa familia zetu, na huduma za afya zinazowafikia wote. Nikipewa ridhaa ya kuwa diwani wenu, nitasimamia kwa karibu miradi ya jamii na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi,” alisema Mahenge huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya uongozi wa kata na wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Tukishirikiana, tutapunguza changamoto zinazotukabili — kama ukosefu wa maji katika baadhi ya vitongoji, upungufu wa madarasa, na vifaa tiba katika zahanati zetu. Mimi siyo mgombea wa maneno, bali wa vitendo,” aliongeza.

Wananchi wa Mji Mwema wamepongeza jitihada za Mahenge na kuonyesha matumaini makubwa kuwa uongozi wake utafungua ukurasa mpya wa maendeleo katika kata hiyo yenye mwelekeo mkubwa wa ukuaji.


Saturday, 11 October 2025

MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA YASISITIZWA KWA WAKULIMA WA MTAA WA MPOBOTA - MJIMWEMA

 

MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA YASISITIZWA KWA WAKULIMA WA MTAA WA MPOBOTA - MJIMWEMA

 

Wakulima wa mtaa wa Mpobota - Mjimwema Halmashauri ya mji Njombe wamesisitizwa kutumia mbolea kwa usahihi na kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2025 na Joshua Ng’ondya kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea nchini, wakati wa kampeni maalum ya kuhamasisha wakulima kuhusu matumizi bora ya mbolea katika wilaya zote za Mkoa wa Njombe ambapo  alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuwajengea wakulima uelewa sahihi kuhusu namna bora ya kutumia mbolea, pamoja na kuwahamasisha kujisajili kwenye daftari la wakulima katika maeneo yao ili kunufaika na ruzuku ya mbolea inayotolewa na serikali.

 


“Tunataka kupata uzoefu kutoka kwa wakulima wa Njombe kwa kuwa wengi wenu hamlimi bila kutumia mbolea. Ni muhimu mjue aina ya mbolea mnazotumia na muwe na taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wake,” alisema Ng’ondya.

 

Akiendelea kuzungumza na wakazi hao alisema serikali kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea wa mwaka 2022/2023 imeendelea kutoa punguzo la bei kati ya Tsh. 60,000 hadi Tsh. 77,000 kutegemeana na umbali kutoka chanzo cha usambazaji wa mbolea.

Aidha, wakulima ambao hawajasajiliwa katika mfumo wa ruzuku wameshauriwa kujipatia namba maalum ya usajili kupitia Maafisa Kilimo wa maeneo yao ili waweze kunufaika na mpango wa ruzuku pamoja na kuwakumbusha wakulima kutunza risiti baada ya kununua mbolea kama uthibitisho wa manunuzi halali, ili kuepuka kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na  zisizo na ubora unaotakiwa.

 

Uwepo wa ruzuku hiyo unalenga kusaidia wakulima katika kukuza uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla, kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani, na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini












Thursday, 9 October 2025

MGOGORO WA ARDHI MAGODA WATATULIWA

 Wataalamu wa Ardhi na Afisa Malalamiko watatua mgogoro wa ardhi wa familia Ngimbuchi, Njombe







Wataalamu wa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe wakiongozwa na Emmanuel Luhamba kwa kushirikiana na Afisa Malalamiko wa Halmashauri, Bi. Eliza Brown, wamefanikiwa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa ardhi uliokuwepo kati ya wanandugu wa familia ya Ngimbuchi Saimoni.


Mgogoro huo uliohusu umiliki wa eneo la ardhi la familia hiyo, lililoko katika eneo la Ekafi, ulihusisha pande mbili zilizokuwa zikivutana kuhusu mipaka na umiliki halali wa shamba la familia.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kufanya upimaji wa eneo husika, wataalamu hao walisaidia kufikia makubaliano ya amani, ambapo kila upande ulipewa ekari moja na nusu (1.5) za ardhi.


Makubaliano hayo yamepokelewa kwa furaha na wanandugu wote, wakiwemo Familia ya Betra Saimoni Ngimbuchi, ambao walisema kuwa suluhisho hilo limeleta utulivu na mshikamano mpya ndani ya familia.


Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Bw. Emmanuel Luhamba alisisitiza umuhimu wa familia na wananchi kwa ujumla kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya mazungumzo na ushirikishwaji wa wataalamu wa ardhi ili kuepuka migogoro isiyo na tija.


Naye Bi. Eliza Brown aliwataka wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kuendelea kufuata taratibu za kisheria katika masuala yote yanayohusiana na ardhi, akibainisha kuwa halmashauri ipo tayari kutoa usaidizi pale panapohitajika.


Kwa hatua hiyo, mgogoro wa familia ya Ngimbuchi umetajwa kuwa mfano mzuri wa utatuzi wa amani wa migogoro ya ardhi kupitia ushirikiano kati ya wananchi na serikali za mitaa.

Thursday, 2 October 2025

WANANCHI MTAA WA KAMBARAGE WAJADILI SHUGHULI ZA MAENDELEO

 Wananchi wa Mtaa wa Kambarage wamekutana kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kujadili shughuli mbalimbali za maendeleo ya mtaa huo.

Lengo kuu la mkutano huu lilikuwa ni kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na kushauriana juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mtaa, Mheshimiwa Fransci Msanga, aliwataka wananchi wote kulinda amani na mshikamano hasa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025. Aidha, aliwaasa wananchi kushirikiana na viongozi wa mtaa katika masuala ya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha usalama unadumishwa.






















Vilevile, Mtendaji wa Mtaa, Ndugu Nicodemas Phuni, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanachangia kwa uaminifu mapato ya mtaa, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika masuala ya afya, lishe bora, usafi wa mazingira na elimu kwa ajili ya kuboresha ustawi wa jamii nzima ya Kambarage.


Kwa pamoja, mkutano uliazimia kuendeleza mshikamano, kuchangia maendeleo, kushirikiana katika usafi wa mazingira na kuhakikisha miradi ya mtaa inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...