Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Njombe TC Wapatiwa Mafunzo ya Lishe Kupunguza Udumavu
Njombe, Septemba 10, 2025 – Wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika Halmashauri ya Mji Njombe wamepatiwa mafunzo maalum ya utekelezaji wa afua za lishe, yakiwa na lengo la kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto na vijana balehe katika mkoa huo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Catholic Relief Services (CRS) kupitia mradi wa Lishe ya Mwanao unaodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Lishe wa Mkoa wa Njombe, Bi. Bertha Nyingu, alisema ni muhimu wahudumu hao kuzingatia matumizi ya virutubisho kwa watoto na vijana wanaowahudumia ili kuhakikisha afya bora na kupunguza athari za lishe duni.
“Tunasisitiza matumizi ya virutubisho kwa watoto na makundi ya balehe kwa sababu wao ndio kundi linalohitaji uangalizi wa karibu. Tukitekeleza afua hizi ipasavyo, tutapiga hatua kubwa kupunguza udumavu mkoani Njombe,” alisema Bi. Nyingu.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo walisema yamewajengea uwezo wa namna bora ya kutoa elimu ya lishe na huduma rafiki kwa jamii. Waliahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa vitendo ili kuboresha afya za watoto na vijana katika maeneo wanayoyahudumia.
Njombe ni miongoni mwa mikoa yenye viwango vya juu vya udumavu nchini, hivyo juhudi za kuimarisha lishe zinaendelea kupewa kipaumbele na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.







No comments:
Post a Comment