Friday, 27 March 2026

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

 

WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika, miundombinu duni ya barabara, upungufu wa viwanda vya kuchakata chai, pamoja na gharama na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Akizungumza katika kikao cha wakulima wa chai kilichowakutanisha viongozi wa AMCOS za chai mkoa huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Chai Mkoa wa Njombe, Engelus Nziku, alieleza kuwa changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wakulima. Alisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa chai, pamoja na kuwajumuisha wakulima katika vikao vya maamuzi vinavyohusu sekta hiyo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Bw. Chrispin Kalinga, alipokea hoja hizo na kuahidi kuzifikisha katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu.

Changamoto kubwa iliyobainishwa ni kuzidiwa kwa uwezo wa kuchakata chai katika Kiwanda cha Kabambe, hali inayowalazimu baadhi ya wakulima kumwaga chai mbichi na kupata hasara kubwa. Hali hiyo imesababisha wakulima wengi kukosa mahali pa kupeleka mazao yao, jambo linalowaathiri kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wakulima hao, juhudi za kuongeza uzalishaji zimezaa matunda, ambapo katika msimu wa 2024/2025 walivuna jumla ya kilo 4,600,000 za chai. Aidha, kuanzia Januari hadi Machi 2026, wastani wa mavuno umefikia tani 70 kwa siku. Hata hivyo, Kiwanda cha Kabambe kinachomilikiwa na mwekezaji anayefahamika kwa jina la Broun kina uwezo wa kuchakata kati ya tani 40 hadi 50 kwa siku, hivyo kusababisha ziada ya tani 20 hadi 30 kushindwa kuchakatwa kila siku.


Kutokana na hali hiyo, wakulima wamelazimika kumwaga chai mbichi, kushindwa kulipa gharama za vibarua, pamoja na kurejesha mikopo ya pembejeo kama mbolea na viuatilifu. Aidha, baadhi yao hulazimika kufanya ukataji wa chai (pruning) kabla ya muda ili kuanza upya uzalishaji, hatua inayosababisha hasara ya mapato kwa msimu mzima.

Wakulima hao wameonya kuwa endapo changamoto hizo hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka, zinaweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya chai na kudhoofisha maisha ya wakulima wengi katika mkoa wa Njombe.

 
















Thursday, 12 February 2026

MZIGO WA MIFUKO 150 YA CHOKAA WAPOKELEWA NA WANACHAMA WA TWENDE PAMOJA AMCOS

 MZIGO WA MIFUKO 150 YA CHOKAA WAPOKELEWA NA WANACHAMA WA TWENDE PAMOJA AMCOS

Wanachama wa Twende Pamoja AMCOS Limited wamepokea mzigo wa mifuko 150 ya chokaa utakaotumika kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza uzalishaji mashambani.

Makabidhiano ya mzigo huo yalifanyika tarehe 11 Februari 2026, ambapo Mwenyekiti wa Bodi, Todos Leonard Msigwa, alipokea mzigo huo kutoka kwa Emmakrata Kyando, Afisa Masoko wa Guavay Company Limited.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, uongozi wa AMCOS ulieleza kuwa upatikanaji wa chokaa hiyo ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto ya tindikali kwenye udongo ambayo imekuwa ikiathiri uzalishaji wa mazao kwa baadhi ya wakulima. Matumizi ya chokaa yanatarajiwa kuongeza rutuba ya udongo, kuboresha afya ya mazao na kuongeza mavuno kwa wanachama.

Aidha, AMCOS imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa pembejeo za kilimo ili kuhakikisha wakulima wanapata huduma na pembejeo bora kwa wakati, hatua itakayosaidia kuongeza tija na kipato kwa wanachama wake.




Monday, 2 February 2026

NJOMBE YAPITIA MBINU SHIRIKISHI ZA KUBORESHA LISHE YA MAMA, WATOTO NA VIJANA BALEHE

 NJOMBE YAPITIA MBINU SHIRIKISHI ZA KUBORESHA LISHE YA MAMA, WATOTO NA VIJANA BALEHE









Tarehe 29 Januari 2026, Mkoa wa Njombe ulifanya kikao cha kupitia na kuchambua mbinu shirikishi za kijamii katika kuboresha lishe ya mama, watoto na vijana balehe. Kikao hicho kililenga kutathmini ufanisi wa afua za lishe zinazotekelezwa na sekta mbalimbali pamoja na kubaini vikwazo vinavyojitokeza katika utekelezaji wake.


Kikao hiki kiliwezeshwa na wadau wa maendeleo CRS na COUNSENUTH kupitia Mradi wa Lishe ya Mwanao, unaofadhiliwa na Serikali ya Norway kupitia UNICEF.


Washiriki wa kikao walitoka katika taasisi na sekta mbalimbali, ikiwemo wataalamu kutoka TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu pamoja na sekta ya Habari na Mawasiliano.


Aidha, taasisi za utafiti na elimu ya juu zilizoshiriki ni pamoja na SUA, TFNC, MUST, NMIST na Ifakara Health Institute. Mashirika ya kiraia yaliyohudhuria ni TAHEA na SANKU, huku wadau wa maendeleo wakiwemo UNICEF, CRS, COUNSENUTH na CUHAS.


Kwa upande wa Mkoa na Halmashauri, washiriki walijumuisha Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa (Ag. RMO), Kaimu Waganga Wakuu wa Wilaya (Ag. DMOs), Maafisa Lishe, waratibu wa lishe shuleni ngazi ya elimu ya msingi na sekondari, Maafisa Kilimo na Mifugo, walimu wawakilishi, Mratibu wa Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) ngazi ya Mkoa pamoja na Afisa Elimu Mratibu wa Lishe ngazi ya Mkoa.


Lengo kuu la kikao hiki lilikuwa kupitia na kuhakiki afua za lishe zinazotekelezwa na sekta mbalimbali ili kubaini ufanisi wake, changamoto zilizopo na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Lishe (NMNAP) pamoja na kuchangia kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG 2 (Kutokomeza Njaa), SDG 3 (Afya Njema) na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira).


@njombe_rs @wizara_afyatz @counsenuth98  @uniceftz @unicef

Sunday, 18 January 2026

Mwenyekiti UVCCM Njombe Aongoza Kikao cha Baraza la Mkoa Kujadili Fursa za Vijana


Mwenyekiti UVCCM Njombe Aongoza Kikao cha Baraza la Mkoa Kujadili Fursa za Vijana













Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Njombe, Ndugu Samwel Mgaya, tarehe 17 Januari 2026 ameongoza kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Njombe kilichofanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu vijana pamoja na mikakati ya kuibua fursa za kiuchumi katika jamii.


Akizungumza wakati wa kikao hicho, Ndugu Mgaya amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za maendeleo, hususan katika maeneo ya ujasiriamali, kilimo cha kisasa, ufundi na matumizi ya teknolojia kama njia ya kujikwamua kiuchumi. 


Ameeleza kuwa UVCCM ina wajibu wa kuwa daraja kati ya serikali na vijana kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo pamoja na namna ya kuzitumia.

Kikao hicho kimejadili pia changamoto zinazowakabili vijana katika mkoa wa Njombe, ikiwemo ukosefu wa ajira, mitaji ya kuanzisha miradi pamoja na uhitaji wa mafunzo ya ujuzi. Wajumbe wa baraza walipata nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na kiuchumi.


Aidha, baraza limeazimia kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu, mafunzo na fursa zitakazowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.


Kikao hicho kimehitimishwa kwa wito kwa viongozi wa UVCCM ngazi zote kuhakikisha wanashuka chini kuwasikiliza vijana, kuhamasisha mshikamano na kuendeleza misingi ya uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

 https://www.facebook.com/share/1GtKoMLdfP/

Thursday, 8 January 2026

UWEKEZAJI WA VITUO VIDOGO VYA MAFUTA WACHOCHEA UCHUMI VIJIJINI NJOMBE

 















NJOMBE: Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Njombe wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi na taratibu za ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo yao, ikiwa ni juhudi za kuchochea maendeleo ya kiuchumi hususan vijijini.

Mafunzo hayo yalitolewa Januari 07, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yakilenga kuwawezesha viongozi hao kusimamia na kuhamasisha uwekezaji salama katika sekta ya mafuta.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Dickson Simkuyu, amesema kuwa kila wilaya ya Mkoa wa Njombe ina vijana walioonyesha nia ya kuanzisha vituo vidogo vya mafuta, ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini kwa kurahisisha upatikanaji wa nishati.

Amesema ujenzi wa vituo hivyo hauhitaji mtaji mkubwa, jambo linalowapa fursa vijana wengi kuingia katika uwekezaji, huku ukichochea ajira na kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini.

“Vituo vidogo vya mafuta vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya vijana na jamii kwa ujumla. Tukiwapatia elimu sahihi kuhusu taratibu na usalama wa ujenzi wake, tunaamini tutapiga hatua kubwa kiuchumi,” amesema Bw. Simkuyu.

Aidha, amesema EWURA itaendelea kutoa semina na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wawekezaji na viongozi katika kila wilaya, kwa lengo la kudhibiti matumizi holela ya mafuta kwa vyombo vya moto na kuhakikisha usalama na ufanisi katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake, Enosy Lupimo, Kaimu Afisa Tarafa wa Tarafa ya Njombe Mjini, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa mpana kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta vijijini, na kuahidi kupeleka elimu hiyo kwa vijana wenye nia ya kuwekeza katika maeneo anayoyasimamia.

Kwa mujibu wa takwimu za EWURA, Mkoa wa Njombe una jumla ya vituo vya mafuta 66, ambapo kati ya hivyo, vituo 8 vinapatikana katika maeneo ya vijijini—hali inayoonesha bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo nje ya maeneo ya mijini.


Wednesday, 17 December 2025

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW) NJOMBE TC WAPIGWA MSASA

 

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW) NJOMBE MJINI WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO 


Wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) Halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kuzingatia miongozo ya utoaji wa huduma jumuishi za Afya,Ustawi wa jamii na Lishe ili kuweza kuimarisha afya za wananchi katika jamii


Wito huo umetolewa disemba 16, 2025 na Bertha Nyigu Afisa Lishe mkoa wa Njombe katika kikao kazi cha kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii Halmashauri ya mji Njombe kupitia mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii-CHWs, ambapo amewataka kutambua utekelezaji wa majukumu yao,kuboresha na kuhamasisha uwekaji wa mipango kazi na utoaji taarifa za utekelezaji wa majukumu yao.


“Unakuta mhudumu wa afya nagzi ya jamii kwenye eneo lililopo badala ya kufanya kazi ,anaacha mpaka tatizo linatokea ,wengine wanahusika na eneo moja na kwa baadhi ya maeneo tumegunduwa wahudumu wengi mmejikita katika usimamizi wa vyoo na mmeacha majukumu mengine ya huduma za afya hasa suala la lishe ambalo kwetu njombe tumekuwa na changamoto,Mafunzo haya yakatubadilishe” Alisema Bertha Afisa Lishe.


Aidha Logato Nziku, Mratibu wa Takwimu Mkoa wa Njombe, aliwahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuzingatia usahihi, uaminifu na ukamilifu katika ukusanyaji wa taarifa za wanazotoa, ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, lishe, ustawi wa kijamii pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa mbalimbali huku akisisitiza takwimu bora ni msingi muhimu katika kuboresha maamuzi ya kisera na mipango ya huduma za afya kuanzia ngazi ya jamii ili kuweza kutumia takwimu hizo kama rejea muhimu katika kutambua changamoto za kiafya na kupanga mikakati ya kukabiliana nazo kwa ufanisi.


Mafunzo hayo yanalenga  kuwajengea uwezo wahudumu  katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuzingatia ukusanyaji sahihi wa takwimu, ufuatiliaji wa huduma na utoaji wa taarifa , uelewa mpana kuhusu umuhimu wa takwimu sahihi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini huduma za afya zinazotolewa katika jamii.


Kikao cha kuwajengea uwezo Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) kuhusu utekelezaji wa afua jumuishi za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kimewezeshwa na Shirika  la Kuhudumia Watoto  Duniani (UNICEF), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono utekelezaji wa Mpango Harakishi na Jumuishi wa Kupunguza Udumavu katika Mkoa wa Njombe.









Tuesday, 2 December 2025

Mratibu wa UKIMWI atoa elimu na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa chuo cha UDOM tawi la Njombe


Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Gladness Sanga, ametoa elimu juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU sambamba na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tawi la Njombe, katika muendelezo wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI.


Zoezi hilo lilitekelezwa Desemba 1, 2025, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo kwa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu:

“Shinda vikwazo, Imarisha mwitikio, Tokomeza UKIMWI.”


Akizungumza na wafanyakazi wa ujenzi pamoja na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo, Bi. Sanga alisema maambukizi mapya ya VVU bado ni changamoto hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo elimu endelevu inahitajika ili kupunguza hatari ya maambukizi.


Kabla ya zoezi hilo, Mratibu huyo alitoa elimu kwa wananchi kupitia redio za Uplands FM na Kings FM, ambapo alisisitiza umuhimu wa kufanya vipimo mara kwa mara, matumizi sahihi ya kondomu, na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.


Katika tukio hilo, mamia ya kondomu ziligawiwa kwa wafanyakazi wa eneo hilo na wakazi jirani kama sehemu ya kuongeza upatikanaji wa kinga na kuwahamasisha kuchukua hatua za kujilinda.









Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili walipongeza juhudi hizo na kuomba kampeni kama hizo ziwe za mara kwa mara, wakisema zinawaongezea uelewa na kuwahimiza kuchukua tahadhari mapema.


Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kusisitiza kuwa itaendeleza juhudi za kuimarisha mwitikio wa jamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI huku ikiweka mkazo katika kupunguza maambukizi mapya na kuhakikisha huduma za ushauri nasaha zinafika kwa makundi yote.

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...