Thursday, 9 October 2025

MGOGORO WA ARDHI MAGODA WATATULIWA

 Wataalamu wa Ardhi na Afisa Malalamiko watatua mgogoro wa ardhi wa familia Ngimbuchi, Njombe







Wataalamu wa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe wakiongozwa na Emmanuel Luhamba kwa kushirikiana na Afisa Malalamiko wa Halmashauri, Bi. Eliza Brown, wamefanikiwa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa ardhi uliokuwepo kati ya wanandugu wa familia ya Ngimbuchi Saimoni.


Mgogoro huo uliohusu umiliki wa eneo la ardhi la familia hiyo, lililoko katika eneo la Ekafi, ulihusisha pande mbili zilizokuwa zikivutana kuhusu mipaka na umiliki halali wa shamba la familia.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kufanya upimaji wa eneo husika, wataalamu hao walisaidia kufikia makubaliano ya amani, ambapo kila upande ulipewa ekari moja na nusu (1.5) za ardhi.


Makubaliano hayo yamepokelewa kwa furaha na wanandugu wote, wakiwemo Familia ya Betra Saimoni Ngimbuchi, ambao walisema kuwa suluhisho hilo limeleta utulivu na mshikamano mpya ndani ya familia.


Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Bw. Emmanuel Luhamba alisisitiza umuhimu wa familia na wananchi kwa ujumla kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya mazungumzo na ushirikishwaji wa wataalamu wa ardhi ili kuepuka migogoro isiyo na tija.


Naye Bi. Eliza Brown aliwataka wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kuendelea kufuata taratibu za kisheria katika masuala yote yanayohusiana na ardhi, akibainisha kuwa halmashauri ipo tayari kutoa usaidizi pale panapohitajika.


Kwa hatua hiyo, mgogoro wa familia ya Ngimbuchi umetajwa kuwa mfano mzuri wa utatuzi wa amani wa migogoro ya ardhi kupitia ushirikiano kati ya wananchi na serikali za mitaa.

No comments:

Post a Comment

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...