Friday, 27 March 2026

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

 

WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika, miundombinu duni ya barabara, upungufu wa viwanda vya kuchakata chai, pamoja na gharama na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Akizungumza katika kikao cha wakulima wa chai kilichowakutanisha viongozi wa AMCOS za chai mkoa huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Chai Mkoa wa Njombe, Engelus Nziku, alieleza kuwa changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wakulima. Alisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa chai, pamoja na kuwajumuisha wakulima katika vikao vya maamuzi vinavyohusu sekta hiyo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Bw. Chrispin Kalinga, alipokea hoja hizo na kuahidi kuzifikisha katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu.

Changamoto kubwa iliyobainishwa ni kuzidiwa kwa uwezo wa kuchakata chai katika Kiwanda cha Kabambe, hali inayowalazimu baadhi ya wakulima kumwaga chai mbichi na kupata hasara kubwa. Hali hiyo imesababisha wakulima wengi kukosa mahali pa kupeleka mazao yao, jambo linalowaathiri kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wakulima hao, juhudi za kuongeza uzalishaji zimezaa matunda, ambapo katika msimu wa 2024/2025 walivuna jumla ya kilo 4,600,000 za chai. Aidha, kuanzia Januari hadi Machi 2026, wastani wa mavuno umefikia tani 70 kwa siku. Hata hivyo, Kiwanda cha Kabambe kinachomilikiwa na mwekezaji anayefahamika kwa jina la Broun kina uwezo wa kuchakata kati ya tani 40 hadi 50 kwa siku, hivyo kusababisha ziada ya tani 20 hadi 30 kushindwa kuchakatwa kila siku.


Kutokana na hali hiyo, wakulima wamelazimika kumwaga chai mbichi, kushindwa kulipa gharama za vibarua, pamoja na kurejesha mikopo ya pembejeo kama mbolea na viuatilifu. Aidha, baadhi yao hulazimika kufanya ukataji wa chai (pruning) kabla ya muda ili kuanza upya uzalishaji, hatua inayosababisha hasara ya mapato kwa msimu mzima.

Wakulima hao wameonya kuwa endapo changamoto hizo hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka, zinaweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya chai na kudhoofisha maisha ya wakulima wengi katika mkoa wa Njombe.

 
















AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...