Wednesday, 17 December 2025

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW) NJOMBE TC WAPIGWA MSASA

 

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW) NJOMBE MJINI WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO 


Wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) Halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kuzingatia miongozo ya utoaji wa huduma jumuishi za Afya,Ustawi wa jamii na Lishe ili kuweza kuimarisha afya za wananchi katika jamii


Wito huo umetolewa disemba 16, 2025 na Bertha Nyigu Afisa Lishe mkoa wa Njombe katika kikao kazi cha kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii Halmashauri ya mji Njombe kupitia mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii-CHWs, ambapo amewataka kutambua utekelezaji wa majukumu yao,kuboresha na kuhamasisha uwekaji wa mipango kazi na utoaji taarifa za utekelezaji wa majukumu yao.


“Unakuta mhudumu wa afya nagzi ya jamii kwenye eneo lililopo badala ya kufanya kazi ,anaacha mpaka tatizo linatokea ,wengine wanahusika na eneo moja na kwa baadhi ya maeneo tumegunduwa wahudumu wengi mmejikita katika usimamizi wa vyoo na mmeacha majukumu mengine ya huduma za afya hasa suala la lishe ambalo kwetu njombe tumekuwa na changamoto,Mafunzo haya yakatubadilishe” Alisema Bertha Afisa Lishe.


Aidha Logato Nziku, Mratibu wa Takwimu Mkoa wa Njombe, aliwahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuzingatia usahihi, uaminifu na ukamilifu katika ukusanyaji wa taarifa za wanazotoa, ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, lishe, ustawi wa kijamii pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa mbalimbali huku akisisitiza takwimu bora ni msingi muhimu katika kuboresha maamuzi ya kisera na mipango ya huduma za afya kuanzia ngazi ya jamii ili kuweza kutumia takwimu hizo kama rejea muhimu katika kutambua changamoto za kiafya na kupanga mikakati ya kukabiliana nazo kwa ufanisi.


Mafunzo hayo yanalenga  kuwajengea uwezo wahudumu  katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuzingatia ukusanyaji sahihi wa takwimu, ufuatiliaji wa huduma na utoaji wa taarifa , uelewa mpana kuhusu umuhimu wa takwimu sahihi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini huduma za afya zinazotolewa katika jamii.


Kikao cha kuwajengea uwezo Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) kuhusu utekelezaji wa afua jumuishi za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kimewezeshwa na Shirika  la Kuhudumia Watoto  Duniani (UNICEF), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono utekelezaji wa Mpango Harakishi na Jumuishi wa Kupunguza Udumavu katika Mkoa wa Njombe.









Tuesday, 2 December 2025

Mratibu wa UKIMWI atoa elimu na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa chuo cha UDOM tawi la Njombe


Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Gladness Sanga, ametoa elimu juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU sambamba na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tawi la Njombe, katika muendelezo wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI.


Zoezi hilo lilitekelezwa Desemba 1, 2025, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo kwa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu:

“Shinda vikwazo, Imarisha mwitikio, Tokomeza UKIMWI.”


Akizungumza na wafanyakazi wa ujenzi pamoja na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo, Bi. Sanga alisema maambukizi mapya ya VVU bado ni changamoto hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo elimu endelevu inahitajika ili kupunguza hatari ya maambukizi.


Kabla ya zoezi hilo, Mratibu huyo alitoa elimu kwa wananchi kupitia redio za Uplands FM na Kings FM, ambapo alisisitiza umuhimu wa kufanya vipimo mara kwa mara, matumizi sahihi ya kondomu, na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.


Katika tukio hilo, mamia ya kondomu ziligawiwa kwa wafanyakazi wa eneo hilo na wakazi jirani kama sehemu ya kuongeza upatikanaji wa kinga na kuwahamasisha kuchukua hatua za kujilinda.









Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili walipongeza juhudi hizo na kuomba kampeni kama hizo ziwe za mara kwa mara, wakisema zinawaongezea uelewa na kuwahimiza kuchukua tahadhari mapema.


Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kusisitiza kuwa itaendeleza juhudi za kuimarisha mwitikio wa jamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI huku ikiweka mkazo katika kupunguza maambukizi mapya na kuhakikisha huduma za ushauri nasaha zinafika kwa makundi yote.

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...