WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO
Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba
serikali pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kuchukua hatua za haraka kutatua
changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika,
miundombinu duni ya barabara, upungufu wa viwanda vya kuchakata chai, pamoja na
gharama na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Akizungumza katika kikao cha wakulima wa chai
kilichowakutanisha viongozi wa AMCOS za chai mkoa huo, Mwenyekiti wa Chama cha
Wakulima wa Chai Mkoa wa Njombe, Engelus Nziku, alieleza kuwa changamoto hizo
zimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wakulima. Alisisitiza umuhimu wa
kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa chai,
pamoja na kuwajumuisha wakulima katika vikao vya maamuzi vinavyohusu sekta
hiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo
la Njombe Mjini, Bw. Chrispin Kalinga, alipokea hoja hizo na kuahidi
kuzifikisha katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Changamoto kubwa iliyobainishwa ni kuzidiwa
kwa uwezo wa kuchakata chai katika Kiwanda cha Kabambe, hali inayowalazimu
baadhi ya wakulima kumwaga chai mbichi na kupata hasara kubwa. Hali hiyo
imesababisha wakulima wengi kukosa mahali pa kupeleka mazao yao, jambo
linalowaathiri kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wakulima hao, juhudi za kuongeza uzalishaji zimezaa matunda, ambapo katika msimu wa 2024/2025 walivuna jumla ya kilo 4,600,000 za chai. Aidha, kuanzia Januari hadi Machi 2026, wastani wa mavuno umefikia tani 70 kwa siku. Hata hivyo, Kiwanda cha Kabambe kinachomilikiwa na mwekezaji anayefahamika kwa jina la Broun kina uwezo wa kuchakata kati ya tani 40 hadi 50 kwa siku, hivyo kusababisha ziada ya tani 20 hadi 30 kushindwa kuchakatwa kila siku.
Kutokana na hali hiyo, wakulima wamelazimika
kumwaga chai mbichi, kushindwa kulipa gharama za vibarua, pamoja na kurejesha
mikopo ya pembejeo kama mbolea na viuatilifu. Aidha, baadhi yao hulazimika
kufanya ukataji wa chai (pruning) kabla ya muda ili kuanza upya uzalishaji,
hatua inayosababisha hasara ya mapato kwa msimu mzima.
Wakulima hao wameonya kuwa endapo changamoto
hizo hazitapatiwa ufumbuzi wa haraka, zinaweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya
chai na kudhoofisha maisha ya wakulima wengi katika mkoa wa Njombe.
















No comments:
Post a Comment