Sunday, 23 March 2025

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA SEKTA YA MISITU

 SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA SEKTA YA MISITU


Na Happiness Shayo - Njombe 


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Misitu ili kuleta ufanisi na manufaa zaidi katika kuchangia ukuaji wa pato la Taifa (GDP) na kunufaisha wananchi kupitia rasilimali za misitu zilizopo hapa nchini.


Ameyasema hayo leo Machi 22, 2025 Mkoani Njombe wakati wa kikao kazi kilichoshirikisha viongozi wa wizara, taasisi na wadau wa sekta ya misitu na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu misitu kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa haraka.


“Sisi kama Serikali tunajivunia Jukwaa hili kwa kuwa kupitia vikao vyake masuala mengi na ya msingi yamepatiwa ufumbuzi. Kwa masuala ambayo pengine nyie wadau mnaona kuwa bado yana ukakasi, naomba kuwahakikishia kuwa Wizara yangu inaendelea kutafuta ufumbuzi wake” amesema Waziri Chana


Waziri Chana amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa sekta hiyo ili kuwasaidia katika kufanya biashara za mazao ya misitu kwa ufanisi huku akiweka mkazo juu ya kupitia na kufanya maboresho kwenye Sheria na Kanuni zilizopo ili kuendana na matakwa ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 kama ilivyotekelezwa hivi karibuni.  


“Tumefanikiwa kufanya mapitio na kuboresha kanuni zinazosimamia utaratibu wa usafirishaji wa Venia kwenda nje ya nchi kwa TSN 807 la mwaka 2024; kanuni za udhibiti na usimamizi wa matumizi ya msumeno wa moto zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na 62 la mwaka 2025; kanuni za mazao na Huduma za Misitu kupitia TSN. 132 la mwaka 2025.”amesema Waziri Chana.







Aidha, Waziri Chana ametolea ufafanuzi juu ya kanuni za jumla za ufugaji Nyuki zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 131 la mwaka 2025 na marekebisho ya kanuni ya uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa mkaa mbadala zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 85 la mwaka 2024.


Katika hatua nyingine Waziri Chana amewahimiza wadau hao kujikita katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu iliyopo hapa nchini ili kuwa na bidhaa zenye thamani ya juu zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira, kuongeza kipato kwa wananchi, wawekezaji na Taifa kwa ujumla kupitia mnyororo wa thamani wa biashara hiyo.


Kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Katibu Mkuu  wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, CP Benedict Wakulyamba, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo Kamishna wa uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wadau na wafanyabiashara wa mazao ya misitu, wakuu wa Taasisi za Wizara kutoka TaFF, TAFORI,TFS na vyuo vya mafunzo, maafisa Waandamizi wa Idara ya Misitu na Nyuki, makamanda wa TFS na wadau wengine ikiwa ni siku moja baada ya Wizara hiyo kuadhimisha siku ya Misitu Duniani na Upandaji miti kitaifa iliyobebwa na kaulimbiu “Ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa rasilimali kwa kizazi hiki na kijacho.”


Saturday, 1 March 2025

SERIKALI MKOANI NJOMBE IMEPIGA MARUFUKU WANANCHI KUTUPA MAKOPO YA MAJI AU YA SODA BARABARANI

 Serikali mkoani Njombe imepiga marufuku wananchi kutupa makopo ya maji au ya soda barabarani na kwenye mifereji na badala yake wayahifadhi katika vifaa maalumu yakiwemo Mapipa,Mifuko na ndoo ili kuweka mazingira katika hali ya usafi.




Katika Maadhimisho ya siku ya Skauti Duniani,Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe, Bi Agatha Mhaiki kwa niaba ya mkuu wa mkoa anawataka wajasiriamali kuzingatia usafi wakati wa uuzaji wa juisi huku wananchi wakitakiwa kuacha tabia ya kutupa makopo njiani.

Ofisa Afya mkoa wa Njombe Saada Milanzi anasema licha ya Skauti kuadhimisha siku yao kwa kufanya usafi katika mtaa wa Idundilanga Mjini Njombe lakini Serikali inaendelea kusisitiza Wananchi kufanya usafi kila Juma Mosi ya mwisho wa mwezi.

Aidha wananchi wa Mjini Njombe mara baada ya kushiriki zoezi la usafi majira ya asubuhi wamesema suala la usafi ni tabia ya mtu hivyo wananchi wenye tabia ya kutoa taka nyumbani na kuzitelekeza kwenye makazi ya watu wanapaswa kukoma mara moja.

Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani, ambayo hufanyika Machi 1  kila mwaka   yalianza kwa kufanya usafi wa mazingira kata ya Njombe Mjini na kuhitimishwa kwa kuzungumza na wananchi  wa Mtaa wa Idundilanga walioshiriki katika shughuli za usafi wa mazingira.










AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...