MATUMIZI
SAHIHI YA MBOLEA YASISITIZWA KWA WAKULIMA WA MTAA WA MPOBOTA - MJIMWEMA
Wakulima
wa mtaa wa Mpobota - Mjimwema Halmashauri ya mji Njombe wamesisitizwa kutumia
mbolea kwa usahihi na kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa kilimo ili kuongeza
tija katika uzalishaji wa mazao.
Wito huo umetolewa
Oktoba 10, 2025 na Joshua Ng’ondya kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa
Mbolea nchini, wakati wa kampeni maalum ya kuhamasisha wakulima kuhusu matumizi
bora ya mbolea katika wilaya zote za Mkoa wa Njombe ambapo alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni
kuwajengea wakulima uelewa sahihi kuhusu namna bora ya kutumia mbolea, pamoja
na kuwahamasisha kujisajili kwenye daftari la wakulima katika maeneo yao ili
kunufaika na ruzuku ya mbolea inayotolewa na serikali.
“Tunataka
kupata uzoefu kutoka kwa wakulima wa Njombe kwa kuwa wengi wenu hamlimi bila
kutumia mbolea. Ni muhimu mjue aina ya mbolea mnazotumia na muwe na taarifa
sahihi kuhusu upatikanaji wake,” alisema Ng’ondya.
Akiendelea
kuzungumza na wakazi hao alisema serikali kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea wa
mwaka 2022/2023 imeendelea kutoa punguzo la bei kati ya Tsh. 60,000 hadi Tsh.
77,000 kutegemeana na umbali kutoka chanzo cha usambazaji wa mbolea.
Aidha,
wakulima ambao hawajasajiliwa katika mfumo wa ruzuku wameshauriwa kujipatia
namba maalum ya usajili kupitia Maafisa Kilimo wa maeneo yao ili waweze
kunufaika na mpango wa ruzuku pamoja na kuwakumbusha wakulima kutunza risiti
baada ya kununua mbolea kama uthibitisho wa manunuzi halali, ili kuepuka
kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na zisizo
na ubora unaotakiwa.
Uwepo wa
ruzuku hiyo unalenga kusaidia wakulima katika kukuza uchumi wa kaya na taifa
kwa ujumla, kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani, na kuhakikisha
upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini











No comments:
Post a Comment