Monday, 25 November 2024

WAZIRI CHANA AINADI CCM MAKAMBAKO, AMTAJA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

 WAZIRI CHANA AINADI CCM MAKAMBAKO, AMTAJA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN 


Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Mhe. Balozi , Dkt. Pindi Chana (Mb) amekinadi Chama cha Mapinduzi huku akiwaomba wananchi kuchagua wagombea wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024.







Ameyasema hayo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Lyamkena, Halmashauri ya Mji wa Makambako Mkoani Njombe leo Novemba 25, 2024.


Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani humo katika Wilaya zote za Makambako, Ludewa, Njombe na Wanging'ombe  za ujenzi wa barabara , shule , vituo vya afya n.k.


Akizungumzia Sekta ya Maliasili na Utalii Mhe. Chana amesema Rais Samia amekuwa kinara katika kutangaza vivutio vya Tanzania hasa kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour.

WEKENI UTARATIBU WA KUSAJILI BIMA MASHAMBA YA MITI- WAZIRI CHANA

WEKENI UTARATIBU WA KUSAJILI BIMA MASHAMBA YA MITI- WAZIRI CHANA










Na Happiness Shayo -Mufindi


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameielekeza Menejimenti ya Shamba la Miti Sao Hill kuweka utaratibu wa kujisajili katika bima kwa lengo la kukabiliana  na hasara zinazotokana na miti kuungua kwa moto.


Waziri Dkt.Chana ameyasema  hayo leo Novemba 25,2024 alipofanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Sao Hill lililopo Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.


"Umefika wakati mkae na Taasisi zinazohusika na Bima za moto ili mjiunge kwa ajili ya kukabiliana na  hasara zinazotokana na matatizo ya moto katika Shamba la Sao Hill”Mhe. Chana amesisitiza.


Aidha, Mhe. Chana ameielekeza Menejimenti hiyo kuendelea kujenga mahusiano mema na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Shamba sambamba na kufanya mikutano na wadau hasa katika Wilaya na Mikoa ili ajenda ya kudhibiti moto iwe ya kudumu.


Katika hatua nyingine Mhe. Chana ameshauri uandaaji wa maandiko ya miradi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya  kisasa vya kudhibiti na kupambana na moto.


Awali, akiwasilisha taarifa ya moto, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, Tebby Yoramu  alisema kuwa moto huo ulitokea tarehe 11 Novemba 2024 na kuathiri eneo la takribani  hekta 69 zenye miti katika shamba la serikali (hekta 17  miti mikubwa na hekta 52 miti midogo) na maeneo mengine yapatayo hekta takribani 430 yaliyokuwa yamevunwa kwa ajili ya maandalizi ya upandaji kwa msimu wa mwezi Januari 2025.


"Kwa upande wa wananchi inakadiriwa eneo la kati ya ekari 150 hadi 200 limeathiriwa na moto huo)” alisema Mhifadhi Tebby.


Katika kukabiliana na changamoto ya matukio ya moto kwenye shamba hilo,  Mhifadhi  Tebby alisema kuwa  mikakati  mbalimbali inaendelea kutekelezwa ikiwemo kuimarisha mahusiano mema na wadau mbalimbali, kuimarisha vikosi vya kudhibiti majanga ya moto kwa kuviongezea ujuzi ,kufanya doria za usiku na mchana, kutumia satellite pamoja na kutenga bajeti ya kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya kutambua na kupambana na moto kama drones.

WAZIRI CHANA ATEMBELEA KITUO CHA MAFUNZO YA MISITU NA VIWANDA VYA MISITU (FWITC)

 WAZIRI CHANA ATEMBELEA KITUO CHA MAFUNZO YA MISITU NA VIWANDA VYA MISITU  (FWITC)






Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) leo Novemba 25, 2024 ametembelea  Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu Mafinga (FWITC- Mafinga) kilichopo Mkoani Iringa na kupokelewa na Mkuu wa Kituo hicho, Berthan Paul Odelo.


Mhe. Chana alikagua karakana ya uzalishaji samani, eneo la mtambo wa kukaushia mbao na kitalu cha miche.


Chuo cha FWITC kinatoa Mafunzo ya Ufundi Stadi katika ngazi ya Astashada NTA Level I-III katika fani za Misitu , Viwanda vya Misitu na Useremala.

Friday, 22 November 2024

WAZIRI CHANA AIPA TANO TTB KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

 WAZIRI CHANA AIPA TANO TTB KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII


Na Happiness Shayo- Dar es Salaam


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameipongeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa jitihada za kutangaza vivutio vya utalii nchini huku akisisitiza kuwa hayo ndio maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza falsafa ya 4R inayojikita katika Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding). 


Ameyasema hayo leo Novemba 22, 2024 wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zilizopo jijini Dar es Salaam.


“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi lakini nasisitiza lazima muwe na ushirikiano katika Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili twende kwa pamoja, muende uwandani na kuvijua vivutio vilivyoko katika taasisi zote” Mhe. Chana amesisitiza.


Aidha, ameweka bayana kuwa Serikali inaitegemea bodi hiyo kuendelea kuingiza mapato hasa fedha za kigeni na kuitaka kutengeneza programu endelevu za muda mrefu za kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi na kuhakikisha tafiti za utalii zinazotolewa zinajulikana kwa taasisi zingine za Serikali ikiwemo Bunge, vyuo vikuu na nyinginezo.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema kuwa TTB imejikita katika vipaumbele kadhaa ikiwemo kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa taasisi hiyo kwa kuwekeza kwenye mali za TTB na kuzalisha mapato kupitia Kituo cha Kutangaza Utalii Kiditali (DDMCC).


Ameongeza, pia TTB itajikita katika kutengeneza mgawanyiko wa kikanda wa maeneo ya vivutio vya utalii na kubuni mazao  mapya ya utalii kama "Boat Cruises" sambamba na mbinu mpya za kutangaza utalii pamoja na kushawishi Waendeshaji wa Biashara ya Utalii kuhusu namna bora ya kuandaaa vifurushi vya utalii ( tourism packages ) ili kupata wageni wengi zaidi.


“ TTB imeimarisha ushirikiano kati yake na wadau mbalimbali kama vile Idara za Wizara na Serikali, Vyombo vya Habari, TRO, Mashirika ya Ndege, Hoteli, Balozi za TZ, vyama vya Utalii, na inaendelea kushawishi uwekezaji katika maeneo ya utalii kama  maeneo ya vivutio (wanyamapori, utamaduni, pwani), huduma za malazi (Hoteli, kambi, Lodge n.k) uwezeshaji wa kufika katika maeneo ya utalii (mashirika ya ndege, usafiri wa ardhini nk), utalii wa matukio  kama MICE Tourism, Vituo vya Burudani, mbuga za mandhari na huduma za kifedha” amesema Bw. Mafuru.



Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi na menejimenti ya TTB.







Tuesday, 19 November 2024

TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII

 TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA SEKTA YA MALIASILI NA UTALII







Na Happiness Shayo- Dar es Salaam


Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Uturuki zimekubaliana kushirikiana kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii lengo ikiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi hizo mbili.


Hayo yamebainika leo Novemba 19,2024 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Mehmet Gulluoglu kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.


Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni ushirikiano kati ya bodi za utalii za Tanzania na Uturuki katika utangazaji wa maeneo  ili kuongeza watalii, kushirikiana na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya kukuza na kuhamasisha watalii kuelekea Tanzania na kuanzisha ubia kwa matukio ya Kimataifa ya Utalii ambayo Bodi ya Utalii Tanzania inaandaa au kushiriki ikiwa ni pamoja na maonyesho ya Swahili International Tourism Expo (S!TE).


Waziri Chana alitumia fursa hiyo kunadi maeneo ya uwekezaji ya Tanzania na kukaribisha wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza katika  huduma za malazi, usafiri na utalii, mashirika ya ndege, biashara ya uendeshaji wa utalii, vituo vya mikutano na uwindaji wa kitalii.


“Napendekeza Tanzania na Uturuki kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi ya nchi hizo mbili ili kuweza kufanya kazi kwa pamoja katika masuala ya biashara ya utalii na uwekezaji” Mhe. Chana amesisitiza.


Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Mehmet Gulluoglu amesema Uturuki iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza Sekta ya Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa Tanzania inavutia na  imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Eliud Mtailuka, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Glory Mndolwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Gwakisa Kamatula.

Monday, 18 November 2024

WAZIRI CHANA AKUTANA NA BALOZI WA URUSI NCHINI TANZANIA

 WAZIRI CHANA AKUTANA NA BALOZI WA URUSI NCHINI TANZANIA


Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan,kuhusu kushirikiana katika Sekta ya Maliasili na Utalii.


Kikao hicho kimefanyika leo Novemba 18,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.


Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa  ni pamoja na umuhimu wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Urusi na Tanzania na kutangaza Tanzania kupitia mawakala wa utalii wa Urusi kwa kuratibu ziara za mafunzo ya utalii (Familiarization Trips).


Pia, kikao kilijadili suala la kushirikiana na kubadilishana ujuzi katika uandaaji wa Maonesho ya kimakumbusho baina  Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Makumbusho ya Urusi.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Urusi katika Taasisi zake zinazohusiana na masuala ya maliasili na utalii huku akisisitiza “Tunataka kutangaza Utalii wa Tanzania duniani kote na Urusi ni mojawapo ya Soko la Watalii”.


Naye, Mhe. Avetisyan alipendekeza kuwa Tanzania itangaze vivutio vya Tanzania kwa soko la Urusi, hasa utalii wa wanyamapori sababu watalii wengi kutoka Urusi wamekuwa wakipendelea zaidi utalii wa fukwe na kwamba nchi zote mbili ziweke mikakati ya pamoja ya masoko ili kuvutia watalii wa Kirusi kuja Tanzania ikiwema kutafsiri filamu ya Royal Tour kwa Kirusi.

Aliongeza kuwa Urusi kwa sasa wako katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya lugha na tamaduni za Kirusi kwa wataalamu wa utalii wa Tanzania  ambapo kwa kuanzia wataanza na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika MWEKA na Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Arusha.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt Florian Mtei, Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Gwakisa Kamatula, Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania ,Vivian Temi na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Bodi ya Utalii Tanzania, Violeth Limbu







Friday, 15 November 2024

GAMONDI AVUNJIWA MKATABA NA YOUNG SC

 Uongozi wa Yanga Sc umethibitisha kuvunja mkataba wa aliyekuwa kocha Mkuu wa kikosi hicho, Angel Miguel Gamondi pamoja na kocha msaidizi, Moussa Ndaw.


Taarifa kutoka klabuni zinaeleza kuwa tayari klabu hiyo imeanza mchakato wa kutafuta Makocha wapya wa kikosi hicho na unatarajiwa kukamilika hivi punde.


Wednesday, 13 November 2024

MKATABA WA UJENZI WA BARABARA KATA NJOMBE MJINI WASAINIWA.

 MKATABA WA UJENZI WA BARABARA KATA NJOMBE MJINI WASAINIWA.



Halmashauri ya Mji Njombe imesaini mkataba na kampuni ya Ubaruku Construction Company Limited (UCCL) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Kata ya Njombe Mjini.
Katika hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Mji Njombe Tarehe 11 Novemba 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Erasto Mpete, aliihimiza kampuni hiyo kutekeleza mradi huo kwa ubora na ufanisi ili kufikia matarajio makubwa ya wananchi.
“Niwaombe mnapoenda kutekeleza mradi huu, mkazingatie makubaliano tuliyokubaliana katika mkataba, na kuhakikisha kuwa ujenzi unafanyika kwa kuzingatia fedha zilizotengwa,” alisema Mhe. Mpete.
Kwa upande wake, Mhandisi Jofrey Dembe kutoka kampuni ya Ubaruku Construction Company Limited aliahidi kutekeleza mradi huo kwa ufanisi na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, kama ilivyoainishwa katika mkataba.
Mradi huo utagharimu shilingi milioni 644,423,650 na utahusisha ujenzi wa barabara za Savanna–Hilliside, Sanga–Pombeshop, Pombeshop–Ngailo, na Kivaa–Mgombela.

Monday, 4 November 2024

Kwaya ya Mt. Yudathadei Yaadhimisha Sherehe Kuu kwa Ustadi na Bashasha

 Kwaya ya Mt. Yudathadei Yaadhimisha Sherehe Kuu kwa Ustadi na Bashasha



Njombe 


Katika mwonekano wa kipekee na shauku kubwa ya kusheherekea siku ya Mtakatifu Yudathadei, Kwaya ya Mt. Yudathadei kutoka Parokia ya Njombe imejipambanua kwa kuandaa sherehe maalum ambayo imewakusanya waumini na wakazi wa eneo hilo kwa lengo la kuhamasisha upendo na mshikamano.


Kwa shauku kuu, Mlezi wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (NACONGO), Joram Hongoli, aliyehudhuria kama mgeni rasmi, wakati akizungumza na cbknews online ameisifia sana kwaya hii kwa jitihada zao za kipekee katika kuhamasisha jamii kusaidia watoto wenye uhitaji wanaosoma katika shule ya msingi ya Kibena. "Kwaya hii si tu imejikita katika kutangaza neno la Mungu, bali pia imeonesha moyo wa huduma na upendo kwa jamii, jambo ambalo ni mfano wa kuigwa," alisema Hongoli.


Kauli mbiu ya sherehe hii, "Kutakuwepo na changizo kwa ajili ya kuwasadia watoto wenye ulemavu wanaopatikana shule ya msingi Kibena," imeonesha kwa kina moyo wa kutoa ambao kwaya ya Mt. Yudathadei imejiwekea. Mbali na maadhimisho hayo, waimbaji wa kwaya hii watatoa burudani kwa umahiri mkubwa, wakijaza ukumbi na nyimbo za sifa na shukrani, huku nyuso za furaha zikiwa zimetawala kwa waumini wote watakaokuwepo baadae kuanzia saa sita mchana wa leo katika ukumbi wa Jimbo la Njombe.


Kwa namna ya pekee, Kwaya ya Mt. Yudathadei imeendelea kuwa taa ya matumaini kwa jamii ya Njombe, ikiwahamasisha wengi si tu kwa nyimbo zao bali pia kwa shughuli mbalimbali za kijamii wanazozifanya. Ni matumaini ya wengi kuwa moyo huu wa huruma na kujali utaendelea kukua na kuleta mabadiliko chanya zaidi kwa jamii ya Njombe.


Kwa hakika, Kwaya ya Mt. Yudathadei imeonesha kuwa muziki wa injili una nguvu ya kuleta mabadiliko – sio tu rohoni bali pia katika hali halisi ya maisha ya watu. Tunawapongeza na tunawatakia kila la kheri katika juhudi zao za kuendeleza huduma hii takatifu! @radiomariatanzania


✍️Hongera kwa kazi nzuri ya kuunga mkono jamii na kwa kuonesha mfano wa upendo na mshikamano.

Friday, 1 November 2024

Wito watolewa kwa Madiwani kuendelea kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

 Wito watolewa kwa Madiwani kuendelea kusimamia  utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.






Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe.Kissa Gwakisa Kasongwa ameendelea kuhimiza madiwani wa Halmashauri ya Mji Mji Njombe, kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia vizuri miradi yote inayoanza pamoja na ile ambayo haijakamilika (miradi viporo) ili iweze kukamilika katika ubora unaotakiwa na kuanza kuwahudumia wananchi.


Akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe ,Bi.Lilian Nyemele Afisa Tarafa,Tarafa ya Njombe Mjini amesema kuwa ni muhimu kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuleta manufaa kwa wananchi.


Aidha aliwakumbusha kuwa msimu wa kilimo unakaribia, hivyo ni jukumu la viongozi na wakulima wote kuhakikisha shughuli za kilimo zinafanyika kwa ufanisi  na endapo changamoto yoyote  itajitokeza itolewe taarifa mapema ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.


Katika jitihada za kuboresha afya ya jamii, amewataka wananchi na viongozi kuendelea kuhamasisha umuhimu wa lishe bora sambamba na kushiriki  siku za lishe, akisema kuwa mikakati thabiti ya lishe itasaidia kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto na kuimarisha afya za wananchi wote.



Wakati Tanzania ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, Mkuu wa wilaya amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi. 


Ameitaka jamii ya Njombe kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama ili kuimarisha amani, kuzuia vurugu, na kuhakikishia kuwa uchaguzi unafanyika kwa utulivu na haki.

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...