Njombe, Oktoba 2025 — Mgombea Udiwani wa Kata ya Mji Mwema kupitia Halmashauri ya Mji Njombe, Ndugu Nestory Mahenge, ameahidi kuleta mabadiliko chanya na ya kweli katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi, ikiwemo elimu, maji safi na salama, pamoja na afya bora kwa wote.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mji Mwema, Ndugu Mahenge alisema kuwa ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi wa kata hiyo ananufaika na huduma bora za kijamii bila upendeleo.
> “Ninaamini maendeleo ya kweli yanaanza na elimu bora kwa watoto wetu, maji safi kwa familia zetu, na huduma za afya zinazowafikia wote. Nikipewa ridhaa ya kuwa diwani wenu, nitasimamia kwa karibu miradi ya jamii na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi,” alisema Mahenge huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya uongozi wa kata na wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Tukishirikiana, tutapunguza changamoto zinazotukabili — kama ukosefu wa maji katika baadhi ya vitongoji, upungufu wa madarasa, na vifaa tiba katika zahanati zetu. Mimi siyo mgombea wa maneno, bali wa vitendo,” aliongeza.
Wananchi wa Mji Mwema wamepongeza jitihada za Mahenge na kuonyesha matumaini makubwa kuwa uongozi wake utafungua ukurasa mpya wa maendeleo katika kata hiyo yenye mwelekeo mkubwa wa ukuaji.












No comments:
Post a Comment