Sunday, 18 January 2026

Mwenyekiti UVCCM Njombe Aongoza Kikao cha Baraza la Mkoa Kujadili Fursa za Vijana


Mwenyekiti UVCCM Njombe Aongoza Kikao cha Baraza la Mkoa Kujadili Fursa za Vijana













Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Njombe, Ndugu Samwel Mgaya, tarehe 17 Januari 2026 ameongoza kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Njombe kilichofanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu vijana pamoja na mikakati ya kuibua fursa za kiuchumi katika jamii.


Akizungumza wakati wa kikao hicho, Ndugu Mgaya amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za maendeleo, hususan katika maeneo ya ujasiriamali, kilimo cha kisasa, ufundi na matumizi ya teknolojia kama njia ya kujikwamua kiuchumi. 


Ameeleza kuwa UVCCM ina wajibu wa kuwa daraja kati ya serikali na vijana kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo pamoja na namna ya kuzitumia.

Kikao hicho kimejadili pia changamoto zinazowakabili vijana katika mkoa wa Njombe, ikiwemo ukosefu wa ajira, mitaji ya kuanzisha miradi pamoja na uhitaji wa mafunzo ya ujuzi. Wajumbe wa baraza walipata nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na kiuchumi.


Aidha, baraza limeazimia kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu, mafunzo na fursa zitakazowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.


Kikao hicho kimehitimishwa kwa wito kwa viongozi wa UVCCM ngazi zote kuhakikisha wanashuka chini kuwasikiliza vijana, kuhamasisha mshikamano na kuendeleza misingi ya uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

 https://www.facebook.com/share/1GtKoMLdfP/

Thursday, 8 January 2026

UWEKEZAJI WA VITUO VIDOGO VYA MAFUTA WACHOCHEA UCHUMI VIJIJINI NJOMBE

 















NJOMBE: Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Njombe wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi na taratibu za ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo yao, ikiwa ni juhudi za kuchochea maendeleo ya kiuchumi hususan vijijini.

Mafunzo hayo yalitolewa Januari 07, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yakilenga kuwawezesha viongozi hao kusimamia na kuhamasisha uwekezaji salama katika sekta ya mafuta.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Dickson Simkuyu, amesema kuwa kila wilaya ya Mkoa wa Njombe ina vijana walioonyesha nia ya kuanzisha vituo vidogo vya mafuta, ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini kwa kurahisisha upatikanaji wa nishati.

Amesema ujenzi wa vituo hivyo hauhitaji mtaji mkubwa, jambo linalowapa fursa vijana wengi kuingia katika uwekezaji, huku ukichochea ajira na kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini.

“Vituo vidogo vya mafuta vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya vijana na jamii kwa ujumla. Tukiwapatia elimu sahihi kuhusu taratibu na usalama wa ujenzi wake, tunaamini tutapiga hatua kubwa kiuchumi,” amesema Bw. Simkuyu.

Aidha, amesema EWURA itaendelea kutoa semina na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wawekezaji na viongozi katika kila wilaya, kwa lengo la kudhibiti matumizi holela ya mafuta kwa vyombo vya moto na kuhakikisha usalama na ufanisi katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake, Enosy Lupimo, Kaimu Afisa Tarafa wa Tarafa ya Njombe Mjini, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa mpana kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta vijijini, na kuahidi kupeleka elimu hiyo kwa vijana wenye nia ya kuwekeza katika maeneo anayoyasimamia.

Kwa mujibu wa takwimu za EWURA, Mkoa wa Njombe una jumla ya vituo vya mafuta 66, ambapo kati ya hivyo, vituo 8 vinapatikana katika maeneo ya vijijini—hali inayoonesha bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo nje ya maeneo ya mijini.


AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...