Tuesday, 2 December 2025

Mratibu wa UKIMWI atoa elimu na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa chuo cha UDOM tawi la Njombe


Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Gladness Sanga, ametoa elimu juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU sambamba na kugawa kondomu katika eneo la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tawi la Njombe, katika muendelezo wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI.


Zoezi hilo lilitekelezwa Desemba 1, 2025, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo kwa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu:

“Shinda vikwazo, Imarisha mwitikio, Tokomeza UKIMWI.”


Akizungumza na wafanyakazi wa ujenzi pamoja na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo, Bi. Sanga alisema maambukizi mapya ya VVU bado ni changamoto hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo elimu endelevu inahitajika ili kupunguza hatari ya maambukizi.


Kabla ya zoezi hilo, Mratibu huyo alitoa elimu kwa wananchi kupitia redio za Uplands FM na Kings FM, ambapo alisisitiza umuhimu wa kufanya vipimo mara kwa mara, matumizi sahihi ya kondomu, na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.


Katika tukio hilo, mamia ya kondomu ziligawiwa kwa wafanyakazi wa eneo hilo na wakazi jirani kama sehemu ya kuongeza upatikanaji wa kinga na kuwahamasisha kuchukua hatua za kujilinda.









Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili walipongeza juhudi hizo na kuomba kampeni kama hizo ziwe za mara kwa mara, wakisema zinawaongezea uelewa na kuwahimiza kuchukua tahadhari mapema.


Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kusisitiza kuwa itaendeleza juhudi za kuimarisha mwitikio wa jamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI huku ikiweka mkazo katika kupunguza maambukizi mapya na kuhakikisha huduma za ushauri nasaha zinafika kwa makundi yote.

No comments:

Post a Comment

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...