NJOMBE: Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Njombe wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi na taratibu za ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo yao, ikiwa ni juhudi za kuchochea maendeleo ya kiuchumi hususan vijijini.
Mafunzo hayo yalitolewa Januari 07, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yakilenga kuwawezesha viongozi hao kusimamia na kuhamasisha uwekezaji salama katika sekta ya mafuta.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Dickson Simkuyu, amesema kuwa kila wilaya ya Mkoa wa Njombe ina vijana walioonyesha nia ya kuanzisha vituo vidogo vya mafuta, ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini kwa kurahisisha upatikanaji wa nishati.
Amesema ujenzi wa vituo hivyo hauhitaji mtaji mkubwa, jambo linalowapa fursa vijana wengi kuingia katika uwekezaji, huku ukichochea ajira na kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini.
“Vituo vidogo vya mafuta vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya vijana na jamii kwa ujumla. Tukiwapatia elimu sahihi kuhusu taratibu na usalama wa ujenzi wake, tunaamini tutapiga hatua kubwa kiuchumi,” amesema Bw. Simkuyu.
Aidha, amesema EWURA itaendelea kutoa semina na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wawekezaji na viongozi katika kila wilaya, kwa lengo la kudhibiti matumizi holela ya mafuta kwa vyombo vya moto na kuhakikisha usalama na ufanisi katika sekta ya nishati.
Kwa upande wake, Enosy Lupimo, Kaimu Afisa Tarafa wa Tarafa ya Njombe Mjini, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa mpana kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta vijijini, na kuahidi kupeleka elimu hiyo kwa vijana wenye nia ya kuwekeza katika maeneo anayoyasimamia.
Kwa mujibu wa takwimu za EWURA, Mkoa wa Njombe una jumla ya vituo vya mafuta 66, ambapo kati ya hivyo, vituo 8 vinapatikana katika maeneo ya vijijini—hali inayoonesha bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo nje ya maeneo ya mijini.


No comments:
Post a Comment