WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW) NJOMBE MJINI WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO
Wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) Halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kuzingatia miongozo ya utoaji wa huduma jumuishi za Afya,Ustawi wa jamii na Lishe ili kuweza kuimarisha afya za wananchi katika jamii
Wito huo umetolewa disemba 16, 2025 na Bertha Nyigu Afisa Lishe mkoa wa Njombe katika kikao kazi cha kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii Halmashauri ya mji Njombe kupitia mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii-CHWs, ambapo amewataka kutambua utekelezaji wa majukumu yao,kuboresha na kuhamasisha uwekaji wa mipango kazi na utoaji taarifa za utekelezaji wa majukumu yao.
“Unakuta mhudumu wa afya nagzi ya jamii kwenye eneo lililopo badala ya kufanya kazi ,anaacha mpaka tatizo linatokea ,wengine wanahusika na eneo moja na kwa baadhi ya maeneo tumegunduwa wahudumu wengi mmejikita katika usimamizi wa vyoo na mmeacha majukumu mengine ya huduma za afya hasa suala la lishe ambalo kwetu njombe tumekuwa na changamoto,Mafunzo haya yakatubadilishe” Alisema Bertha Afisa Lishe.
Aidha Logato Nziku, Mratibu wa Takwimu Mkoa wa Njombe, aliwahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuzingatia usahihi, uaminifu na ukamilifu katika ukusanyaji wa taarifa za wanazotoa, ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, lishe, ustawi wa kijamii pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa mbalimbali huku akisisitiza takwimu bora ni msingi muhimu katika kuboresha maamuzi ya kisera na mipango ya huduma za afya kuanzia ngazi ya jamii ili kuweza kutumia takwimu hizo kama rejea muhimu katika kutambua changamoto za kiafya na kupanga mikakati ya kukabiliana nazo kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wahudumu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuzingatia ukusanyaji sahihi wa takwimu, ufuatiliaji wa huduma na utoaji wa taarifa , uelewa mpana kuhusu umuhimu wa takwimu sahihi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini huduma za afya zinazotolewa katika jamii.
Kikao cha kuwajengea uwezo Wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) kuhusu utekelezaji wa afua jumuishi za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kimewezeshwa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono utekelezaji wa Mpango Harakishi na Jumuishi wa Kupunguza Udumavu katika Mkoa wa Njombe.







No comments:
Post a Comment