Kikundi cha Lunyanywi Fish Farm chashiriki kikamilifu kusikiliza kero za wananchi kwa siku nne mfululizo
Kikundi cha Lunyanywi Fish Farm kimekuwa miongoni mwa taasisi na vikundi vilivyoshiriki kikamilifu katika zoezi la kusikiliza kero za wananchi lililoratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe. Zoezi hilo limefanyika kwa muda wa siku nne mfululizo katika eneo la stendi ya zamani mjini Njombe.
Lengo kuu la zoezi hilo ni kuwapa wananchi jukwaa la wazi kueleza changamoto, malalamiko na mapendekezo yao kuhusu huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiutawala, huku taasisi na mashirika mbalimbali yakishiriki kusikiliza na kutoa mrejesho wa haraka.
Kikundi cha Lunyanywi Fish Farm kimeeleza kuwa kushiriki kwake katika zoezi hilo ni sehemu ya wajibu wao wa kijamii na nia ya dhati ya kushirikiana na serikali na wananchi kuboresha maisha ya jamii inayowazunguka kuhusu ufugaji wa samaki .
Wawakilishi wa kikundi hicho kinachoongozwa na Mussa Lupenza ameelezea kuwa wamepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chakula cha samaki, na changamoto zinazowakabili wafugaji wa samaki wadogo wadogo katika mji wa Njombe.
“Tumejifunza mengi kutoka kwa wananchi. Wameeleza kiu yao ya kupata mafunzo ya ufugaji bora wa samaki, upatikanaji wa vifaranga na masoko ya uhakika. Sisi kama Lunyanywi Fish Farm tupo tayari kushirikiana nao katika kutatua changamoto hizi.” Alisema Mussa Lupenza
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya kilimo ,mifugo ma Uvuvi Thadei Luoga kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, alilipongeza kundi hilo kwa ushiriki wao na kuwataka wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano huo wa kuwafikia wananchi moja kwa moja.
Zoezi hilo la kusikiliza kero limeonekana kuleta matumaini kwa wakazi wa Njombe, ambao wameeleza kufurahishwa na usikivu na mwitikio wa taasisi na vikundi vinavyoshiriki.



No comments:
Post a Comment