Saturday, 12 April 2025

Maofisa Watendaji, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa Njombe TC Wapatiwa Mafunzo ya Kutokomeza Udumavu



Njombe, Aprili 12, 2025 – Maofisa Watendaji wa Kata, Watendaji wa Mitaa na Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wote wa Halmashauri ya Mji wa Njombe wamepatiwa mafunzo maalum yenye lengo la kutokomeza tatizo la udumavu katika maeneo yao. 

Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na Shirika la Catholic Relief Services (CRS) na Centre for Counselling, Nutrition and Health Care (COUNSENUTH), kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF), chini ya mradi wa Lishe ya Mwanao.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Aprili 12, 2025,katika Ukumbi wa Nazareth Mjini Njombe Afisa Lishe wa Mkoa wa Njombe, Bi. Betha Nyigu, alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kushirikiana kwa karibu na wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kusimamia utekelezaji wa afua za lishe. Alisema kuwa udumavu ni changamoto kubwa inayoukabili mkoa wa Njombe, na juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira yenye lishe bora.


"Ni jukumu letu kama viongozi wa kijamii kuhakikisha tunalifikia kila kaya na kuhakikisha elimu ya lishe inafika kwa wananchi wetu. Kupitia ushirikiano na wahudumu wa afya, tunaweza kuhakikisha watoto wetu wanapata lishe stahiki na hivyo kupunguza viwango vya udumavu vinavyoathiri maendeleo ya watoto kimwili na kiakili," alisema Bi. Nyigu.




Kwa upande wake, Bi. Amina Ramadhani, Afisa Lishe kutoka Centre for Counselling, Nutrition and Health Care (COUNSENUTH), alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa na maarifa kuhusu lishe bora katika familia, shule na jamii kwa ujumla. Alifafanua kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kuimarisha uelewa wa vijana hususan wa rika balehe, pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kutumia walimu kama mabalozi wa lishe mashuleni.


"Mradi huu unalenga pia kuhakikisha taarifa muhimu za lishe zinapatikana kutoka sekta mbalimbali kwa wakati, kupitia mfumo wa utoaji taarifa wa kila robo mwaka. Pia tunasisitiza lishe jumuishi inayoangazia mahitaji ya kijinsia, kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika mapambano dhidi ya udumavu," alisema Bi. Amina.



Kupitia mafunzo haya, viongozi wa jamii wamewezeshwa kwa ujuzi wa kuibua changamoto zinazochangia udumavu na kuzipatia suluhisho kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, wazazi na walezi, huku wakitumia rasilimali zilizopo katika ngazi ya jamii.


Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa viwango vya udumavu nchini Tanzania, hali inayohusishwa na upungufu wa lishe bora katika familia nyingi. Mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu lishe na kuchukua hatua stahiki kwa ustawi wa kizazi kijacho.





No comments:

Post a Comment

AKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO

  WAKULIMA WA CHAI NJOMBE WAIBUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU NA SOKO Wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wameiomba serikali pamoja na wada...