Kamati ya Siasa Utalingolo Yapongeza Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
https://www.instagram.com/p/DI4w7Y6M0E0/?igsh=aDYzb3RhdThjZG42
NJOMBE-Na Mwandishi wetu.
Aprili 25, 2025 – Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Utalingolo imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo, ikisema kuwa juhudi zinazofanywa na wataalam wa halmashauri ni uthibitisho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Utalingolo, Ndugu Beniginus Myonga, akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi leo, amesema miradi hiyo ni ya muhimu kwa ustawi wa wananchi na inaonesha namna serikali inavyojitoa katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
"Tunashukuru sana kwa namna miradi hii inavyotekelezwa. Hii ni kazi nzuri inayopaswa kupongezwa. Tunaona kabisa utekelezaji wa Ilani ya CCM unavyoendelea kwa ufanisi," alisema Myonga.
Pamoja na pongezi hizo, Myonga alimtaka Mheshimiwa Diwani wa kata hiyo kuhakikisha anasimamia kikamilifu miradi ambayo haijakamilika, kwa kufuatilia upatikanaji wa fedha kutoka halmashauri ili miradi hiyo iweze kukamilishwa kwa wakati.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya Siasa walipongeza jitihada za serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa serikali na wataalam ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
Kamati hiyo ilitembelea vijiji vyote vya kata ya Utalingolo ambapo miradi ya elimu, afya, na miundombinu inatekelezwa kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuleta maendeleo ya karibu kwa wananchi.











No comments:
Post a Comment