NJOMBE: Mwanahabari Prosper Mfugale Ajitosa Kugombea Udiwani Kata ya Ihanga Kupitia CCM
Juni 29, 2025 Mwandishi wa habari wa vituo vya Tumaini TV na Njombe TV, Prosper Mfugale, amejiunga rasmi katika ulingo wa siasa baada ya kuchukua fomu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya udiwani wa Kata ya Ihanga, iliyopo katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Mfugale, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele katika kuripoti masuala ya kijamii na maendeleo mkoani Njombe, amesema uamuzi wake wa kuingia kwenye siasa umetokana na dhamira ya dhati ya kutumia maarifa na uzoefu wake kusaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wa Ihanga.
"Nimekuwa karibu na wananchi kwa miaka mingi kupitia kazi yangu ya uandishi wa habari. Najua changamoto zao na ninayo nia ya dhati ya kuzitatua kwa kushirikiana nao," amesema Mfugale mara baada ya kuchukua fomu.
Hatua yake imeibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa kata hiyo, ambapo wengi wamepongeza uamuzi huo, wakimtaja kama kijana mwenye maono, anayeielewa jamii na anayestahili nafasi ya uongozi kwa sababu ya ukaribu wake na wananchi.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM unaendelea kote nchini, huku ukitarajiwa kuibua majina mapya ya watumishi wa umma, wanahabari, na wanajamii wenye dhamira ya kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao.





No comments:
Post a Comment