Shirika la Railway Children Africa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Njombe limezindua rasmi Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii katika Stendi Kuu ya Mabasi Njombe, likiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto na makundi mengine yaliyo hatarini unazingatiwa.
Akizungumza juni 20,2025 katika uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Gabriel Kulaba, amewataka wananchi na wafanyabiashara wa stendi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa huduma muhimu sasa zimesogezwa karibu nao.
Akielezea umuhimu wa dawati hilo, Subira Mshana Mwakilishi wa shirika la Railway Children Africa wamesisitiza kuwa hii ni hatua ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Madawati ya Huduma za Ustawi wa Jamii katika Vituo vya Usafiri.
“Tunataka kuhakikisha kila mtoto na mwananchi aliyopo katika maeneo ya stendi anapata huduma stahiki kwa wakati, bila kujali mazingira aliyopo pasipokufanyiwa unyanyasaji ,” Alisema Subira Mshana.
Mradi huo umefadhiliwa na shirika la Railway Children Africa kwa lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika maeneo ya umma, hasa vituo vya usafiri kama stendi Kupitia dawati hilo, jamii itapata huduma za ushauri, ulinzi, na msaada wa haraka kwa watoto walioko katika mazingira hatarishi.
Dawati hilo pia litakuwa na Kamati Maalum itakayofuatilia kwa karibu matukio ya ukatili, kutoa taarifa, na kuratibu misaada ya dharura kwa watoto walioko hatarini. Aidha, jamii imetakiwa kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa na kusaidia juhudi hizi kwa moyo wa kujitolea.
shirika la Railway Children Africa limeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa stendi ya Njombe inakuwa mfano wa kuigwa kama eneo salama na rafiki kwa watoto na makundi mengine maalum.

No comments:
Post a Comment